Imebainika kuwa waathirika wa magonjwa adimu wanakabiliwa na gharama kubwa za matibabu, hali inayofanya upatikanaji wa tiba kuwa changamoto kubwa kwao na familia zao.
Kwa mujibu wa Prof. Francis Furia, kutoka Chuo cha Sayansi na Tiba Shirikishi Muhimbili (MUHAS) wakati wa maadhimisho ya siku ya magonjwa adimu duniani amefafanua kuwa mgonjwa wa ugonjwa adimu anaweza kuhitaji matibabu ya gharama kubwa kwa muda mrefu, jambo linalofanya baadhi yao kushindwa kuendelea na tiba.
"Sindano moja ya matibabu inagharimu dola 2,000, na mgonjwa anahitaji moja kila wiki. Gharama hizi ni mzigo mzito, lakini kwa mshikamano wetu, tunaweza kuleta mabadiliko na kuhakikisha kila mgonjwa anapata matibabu anayohitaji," alisema Prof. Furia.
Mara nyingi, wagonjwa wanakosa bima ya afya inayoweza kugharamia matibabu yao, na hivyo kulazimika kutegemea michango ya jamii au misaada ya taasisi mbalimbali.
Takwimu za kimataifa zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya magonjwa adimu husababisha athari mbaya zaidi kwa wananchi wengi wenye kipato cha chini. Kwa kuwa tafiti juu ya magonjwa haya ni chache, dawa nyingi zinazotengenezwa kwa ajili ya tiba huwa na gharama kubwa kutokana na ugumu wa uzalishaji wake.